SERIKALI KUANZISHA MALIPO YA LESENI KWA MTANDAO - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Tuesday, 17 August 2021

SERIKALI KUANZISHA MALIPO YA LESENI KWA MTANDAO






Na Richard Mwaikenda, Dodoma.
SERIKALI iko mbioni kunzisha mpango wa malipo ya maombi ya biashara kwa njia ya mtandao. Mpango huo umetangazwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) Godfrey Nyaisa wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya maafisa Biashara kutoka mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida, jijini Dodoma.

Amesema kuwa lengo la mpango huo ni kurahisisha utendaji Kazi na kuwadhibiti maafisa wabadhilifu wa fedha za umma ambao baadhi walikuwa wanajitengenezea vitabu feki vya leseni.

Nyaisa amesema kuwa hivi sasa maombi yote ya leseni yatakuwa kwenye mfumo mmoja ambapo mfanyabiashara atakuwa anaomba leseni kupitia kwenye mtandao na kulipia kwa kutumia namba maalumu ya malipo serikalini (Control Number) na kwamba mpango huo utapunguza kwa asilimia kubwa ubadhirifu hivyo kuongeza wigo wa mapato.

Amewaonya waliokuwa na tabia hiyo ya ubadhilifu kuachana nayo na kinachotakiwa ni kujipanga upya kuchapa kazi ya kuhakikisha katika maeneo yao wanaongeza wigo wa kurasimisha wafanyabiashara ili serikali iwe inaongeza mapato.

"Inatakiwa Afisa Biashara atengeneze Kanzi Data (Database) ya idadi ya wafanyabiashara waliopo katika eneo lake itasaidia sana kurahisisha utendaji kazi. Msikurupuke sana kufunga biashara, hivi ukifunga wewe unategemea nini, hujui unachangia kuuaq uchumi wa nchi?" Alihoji Nyaisa.

"Serikali ina shida na mfanyabiashara na mfanyabiashara ana shida hivyo msikurupuke kuwafungia biashara, kaeni muelewane, mtumie busara lakini pia mkae mkijuwa kuwa licha ya Serikali kutaka mapato lakini kazi yake kubwa ni kutoa huduma," amesema Nyaisa.

Aidha ametaka maafisa biashara kuwajengea mazingira mazuri wawekezaji wanaokwenda katika maeneo yao, badala ya kuwatendea mambo yasiyofaa yanayowakatisha tamaa ikiwemo kuwaomba rushwa.

Malengo ya mafunzo hayo kwa maafisa biashara ni; kuboresha utoaji wa huduma za leseni, kujua majukumu yao, kuwa na mfumo wa ufanyazi kazi wa pamoja pia wawe wawezeshaji badala ya kuwa wababe kwa wafanyabiashara.

Inatakiwa kubadili fikra na mtazamo kwa wafanyabiashara na kutumika kama chachu ya uanzishwaji wa biashara katika maeneo yao.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso