Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe.Amos Makalla akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mfumo wa ulipaji ada ya maegesho kwa njia za kielektroniki kwenye mkoa huo leo tarehe 24/08/2021.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe.Amos Makalla akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa mfumo wa ulipaji ada kwa njia za kieletroniki leo tarehe 24/08/2021.
Mkuu aa Kitengo cha TEHAMA kutoka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA), Bw.Stanley Mlula akiongea na waandishi wa habari kueleza namna mfumo wa ulipaji ada ya maegesho kwa njia za kielektroniki unavyofanya kazi na njia za kufanya malipo katika mfumo huo leo tarehe 24/08/2021.
******************
Ikiwa ni katika kuendena sawa na mabadiliko ya sayansi na teknolojia sanjari na uboreshaji wa huduma kwa wananchi na kuisaidia serikali katika suala la udhibiti wa mapato, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umetambulisha rasmi Mfumo wa Ulipaji Ada ya Maegesho kwa Njia za Kielektroniki.
Mfumo huo wenye faida luluki, unatarajiwa kuanza kazi rasmi katika Mkoa wa Dar es Salaam Septemba Mosi, mwaka huu, mfumo ambao unakwenda kutatua changamoto zilizokuwepo katika ukusanyaji wa ushuru wa maegesho katika barabara za Mkoa wa Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla leo Jumanne Agosti 24, 2021 wakati wa uzinduzi rasmi wa mfumo huo ambapo amesema mfumo huo unakwenda kuongeza mapato kwa kudhibiti uvujaji wa mapato ya serikali.
Makalla ameongeza kuwa, kutokana na Jiji la Dar es Salaam kuw kubwa na kuongoza kibiashara ukubwa huo unapaswa kwenda sanjari na urahisi katika kupata huduma ikiwemo huduma ya ulipaji wa ada za maegesho.
“Jiji la Dar es Salaam ni jiji kubwa la la kibiashara lenye watu wengi, tusingependa watu wapate usumbufu, hivyo tumeamua kuja na mfumo huu wa kulipa ada ya maegesho kwa njia za Kielektroniki ili kurahisisha huduma kwao” alisema Makalla na kuongeza
“Mfumo wa ulipaji ada ya maegesho kwa njia za Kielektroniki utaanza Septemba Mosi, 2021, mfumo huu unakwenda kutatua changamoto zilizokuwepo katika ukusanyaji ushuru wa maegesho katika barabara za TARURA”
Akielezea faida za mfumo huo, Makalla amesema pamoja na mambo mengine unahakikisha usalama wa mapato kufika serikalini lakini kubwa zaidi kuondoa wasiohusika katika ukusanyaji kujinufaisha kupitia ushuru wanaokusanya maarufu vishoka wa parking
“Kulikuwepo na watu ambao si wafanyakazi wa TARURA wala jiji wala Manispaa, ambao walijianzishia utaratibu wa ukusanyaji mapato lakini mapato hayo yanaishia mikononi mwao ambao jina maarufu ni ‘vishoka wa parking’. Mfumo wa ulipaji ada za maegesho kwa njia za Kielektroniki ni mwarobaini kwa watu hao” aliongeza Makalla
Naye Mkuu wa kitengo cha TEHAMA kutoka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Stanley Mlula amesema, mfumo wa ulipaji ada ya maegesho kwa njia za Kielektroniki umeshaanza kufanya kazi katika mikoa ya Iringa, Dodoma, Mwanza na Singida na kote huko umeonesha matokeo mazuri na makubwa huku lengo kubwa likiwa ni kuisaidia serikali katika kudhibiti mapato yake na kurahisisha huduma kwa wananchi.
Akielezea njia za ulipaji, Mlula amefafanua kuwa, ulipaji wa ada za maegesho kupitia mfumo huo utafanyika kwa njia ya mitandao ya simu, benki na njia zote za ulipaji fedha kidijitali.
Mfumo wa Ulipaji Ada ya Maegesho kwa Njia za Kielektroniki (TeRMIS) ambao ni umebuniwa na wataalamu wa ndani kutoka TARURA ni kielelezo tosha kwamba, wataalamu wa ndani ya nchi wana uwezo mkubwa katika kubuni na kutengeneza mifumo itakayosaidia Taifa katika utatuzi wa changamoto mbalimbali.
No comments:
Post a Comment