SHILINGI BILIONI MOJA KUKAMILISHA CHUO KIKUU ZANZIBAR - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday, 10 July 2021

SHILINGI BILIONI MOJA KUKAMILISHA CHUO KIKUU ZANZIBAR

 


Serikali imetenga zaidi ya Shilingi Bilioni Moja kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa majengo katika Taasisi ya Sayansi za Bahari ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam iliyopo Buyu,Zanzibar.

Akizungumza baada ya kukagua chuo hicho Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Profesa Joyce Ndalichako, alisema Wizara kupitia mradi wa Kuendeleza Elimu ya Juu tayari imeshatenga kiasi hicho cha pesa kwa ajili ya ujenzi wa mabweni katika Taasisi hiyo.

Waziri Ndalichako alisema mbali ya fedha hizo Wizara imeshaanza kufanya mapitio ya miradi yake ili kuona namna ya kupata fedha za kumalizia ujenzi wa majengo ambayo tayari misingi yake imeshajengwa na imekaa muda mrefu bila kukamilishwa.

“ Serikali haiwezi kuona fedha zilizotumika kujenga misingi hii zikipotea bure kwa kukosekana fedha za kukamilisha ujenzi,lazima tufanye jitihada kukamilisha,”alisema Profesa Ndalichako.

Alibainisha kwamba matamanio yake ni kuona majengo hayo yanaanza kujengwa katika mwaka 2021/22 na kukamilika mwaka 2022/23 ili madhumuni ya kuanzishwa kwa Taasisi hiyo yafikiwe ikiwa pamoja na kutekeleza sera ya uchumi wa bluu.

Aidha, aliupongeza uongozi wa Taasisi hiyo kwa kuanza masomo pamoja na kuwa na changamoto mbalimbali, amezisitiza kuwa chuo hicho kinatekeleza maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania   Samia Suluhu Hassan juu ya kuandaa vijana wenye ujuzi.

Katika kutekeleza maono hayo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Taassisi hiyo imeanzisha Programu za mafunzo mbalimbali ambayo yanatoa ujuzi katika tasnia ya Sayansi ya Bahari.

Naye Mbunge wa Kiembe Samaki ambapo Taasisi hiyo ipo Mhe. Mohammed Maulid amemshukuru Waziri kwa kufika katika Taasisi hiyo ambayo ni tegemeo kubwa kwa taifa katika kuandaa wataalamu wa sayansi ya majini ambao wataiwezesha kufanikisha uchumi wa bluu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Sayansi za Bahari Dkt.Magreth Kyewalyanga alimwambia waziri kuwa ili kukamilisha ujenzi wa miundombinu iliyo kwenye hatua ya msingi zinahitajika kiasi cha shilingi bilioni saba na milioni mia tano.

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Serikali ya wanafunzi DARUSO Frank Buluma alisema Taasisi hiyo imewasaidia wao kama vijana kupata fursa ya kupata elimu ya Sayansi ambayo itawawezesha kushiriki katika kukuza uchumi kupitia uchumi wa bluu. Ametoa wito kwa vijana kujiunga na chuo hicho ambacho kitawawezesha kupata elimu itakayowasaidia kujiajiri katika eneo jipya la ajira.

 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso