MAKATIBU WA KUU WA SADC WA MASUALA YA FEDHA WAJADILI KUHUSU UKUAJI WA UCHUMI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Tuesday, 13 July 2021

MAKATIBU WA KUU WA SADC WA MASUALA YA FEDHA WAJADILI KUHUSU UKUAJI WA UCHUMI





Makatibu Wakuu wa masuala ya Fedha na Uwekezaji wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wameanza kikao cha siku mbili kinachoangazia pamoja na mambo mengine uanzishwaji wa mfuko wa fedha wa SADC na kupitia ripoti za nyuma ikiwa ni maandalizi ya kikao cha Mawaziri kitakachofanyika tarehe 15 Julai, 2021.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban, ambaye ameongoza ujumbe kutoka Tanzania kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Emmanuel Tutuba, alisema kuwa wameanza kwa kuangazia masuala ya fedha na namna ya kukuza uchumi wa nchi wanachama.

Bi. Amina Shaaban alisema kuwa miongoni mwa ajenda za kikao hicho ni pamoja na kuangalia utekelezaji wa ripoti za nyuma, ripoti za Gavana wa Benki Kuu na uanzishwaji wa Mfuko wa Maendeleo wa SADC.

Ameeleza kuwa ajenda hizo ni muhimu katika maendeleo ya Tanzania katika sekta mbalimbali za kukuza uchumi, hivyo kama nchi inashiriki kikamilifu.

Aidha Mawaziri wenye dhamana na masuala ya Fedha na Uwekezaji na Magavana wa Benki Kuu kutoka nchi 16 wanachama wa SADC watafanya kikao cha kujadili masuala ya Fedha na Uwekezaji pamoja na kupokea taarifa ya utekelezaji wa maamuzi yaliyotolewa na Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji katika mkutano uliofanyika mwezi Julai 2020, Dar es Salaam, Tanzania.

Mkutano huo wa Mawaziri utafanyika chini ya Mwenyekiti Waziri wa Uchumi na Fedha wa Msumbiji Mhe. Adriano Afonso Maleiane.

Vilevile mkutano huo wa Mawaziri utajadili kwa kina na kutoa maamuzi ya kisera kuhusu athari za Kiuchumi na Kijamii za COVID-19 pamoja na mambo mengine kadhaa.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa Mawaziri wenye dhamana na masuala ya Fedha na Uwekezaji na Magavana wa Benki Kuu kutoka nchi 16 wanachama wa SADC utaeleza maadhimo waliyokubaliana katika kikao hicho kama nchi ambapo kwa upande wa Tanzania utaongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso