Serikali
imetoa agizo kwa kwa Kampuni za Simu sambamba na Wamiliki wa Minara ya
Mawasiliano,kuhakikisha inaingia mikataba ya ulinzi wa minara ya mawasiliano
yao na serikali za vijiji za eneo husika.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew,katika ziara yake ya kikazi katika Wilaya ya Newala mkoani Mtwara ya kukagua ujenzi, uwezo na ubora wa minara ya mawasiliano.
Kauli hiyo ilikuja baada ya kukutana na malalamiko ya malipo ya mlinzi katika mnara wa tigo uliopo Kijijini Mdimba pamoja na changamoto ya mawasiliano ya mtandao wa tigo kutokana na mnara huo kutumia nishati ya mwanga wa jua pekee.
Sambamba na hilo, Mhandisi Kundo alitoa agizo kwa Wakuu wa Wilaya nchini kuhakikisha mtoa huduma yeyote mwenye mnara wa mawasiliano ndani ya wilaya zao anaandikiwa barua ya kufanya makubaliano mapya na kusaninisha mikataba ya ulinzi wa minara.
“Kuanzia sasa watoa huduma wote watakuwa wanaingia mikataba ya ulinzi wa minara na Serikali ya Kijiji husika ambayo ndio itawajibika kuhakikisha eneo la mnara linakuwa na ulinzi muda wote,”alisema Naibu Waziri huyo.
Alifafanua kuwa. “ utaratibu huu umekuwa ukitumiwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) bila kuleta changamoto wala malalamiko ya aina yeyote.”
Katika hatua nyingine Mhandisi Kundo ametoa miezi mitatu kwa kampuni ya simu ya tigo kuhakikisha imefikisha nishati ya umeme katika mnara wa mawasiliano wa kampuni hiyo uliopo katika kijiji cha Mdimba unaotumia nishati ya mwanga wa jua pekee wakati nishati ya umeme imekwishafika kijijini hapo
Aidha, katika ziara yake wilayani Newala,Mhandisi Kundo, alifanya ufuatiliaji wa minara ya mawasiliano ya kampuni ya simu ya Halotel iliyopaswa kujengwa kwa ruzuku kutoka Serikalini kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na kukuta hakuna ujenzi uliofanyika.
Alidai mkataba wa ujenzi wa mnara wa Halotel katika kijiji cha Chilangala ulisainiwa toka Januari, 2020 na utekelezaji wake ulikuwa wa miezi 9 lakini hakuna utekelezaji wowote uliofanyika.
Hivyo Mhandisi Kundo aliagiza UCSAF kufanya ufuatiliaji wa minara hiyo na kuhakikisha imejengwa,vinginevyo fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi huo zirejeshwe UCSAF na stakabadhi ya kurejesha fedha hizo ziwasilishwe sehemu husika kwa uthibitisho.
Aliongeza kuwa mradi huo una sintofahamu nyingi kwasababu mtandao wa Halotel tayari unapatikana katika eneo husika wakati jukumu la msingi la Mfuko huo ni kufikisha mawasiliano katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma ya mawasiliano.
Naye Mbunge wa Newala Vijijini,Maimuna Mtanda, alitoa rai kwa watendaji wa Serikali waliopewa dhamana ya kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo hususan miradi ya mawasiliano kuwajibika ipasavyo kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma yenye kiwango kilichokusudiwa.
Akizungumza katika ziara hiyo Mkuu wa wilaya ya Newala,Mwangi Kundya,alisema kuwa amepokea maelekezo yanayohusu Wilaya na Kamati ya Ulinzi na Usalama na kuahidi yatafanyiwa kazi kwa kuchukua hatua Madhubuti na kwa wakati ili kuhakikisha kero na malalamiko ya wananchi kuhusu mawasiliano yanapatiwa majibu.
No comments:
Post a Comment