Watu wanne wamefariki dunia katika ajali ya basi Kampuni ya Classic lenye namba za usajili binafsi Salum Rashidi Classic (SRC 3), likitokea Kampala nchini Uganda kwenda Jijini Dar es salaam.
Ajali hiyo imetokea leo majira ya saa 10 alfajiri katika Kona ya Didia wilayani Shinyanga, na kusababisha vifo vya abiria hao na majeruhi 20, ambapo wanapatiwa matibabu hospitalini.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga ACP Debora Magiligimba, amewataja watu waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni Wahida Yusuph mkazi wa Pemba, Joseph Joseph mkazi wa Dar es salaam, Rehema Haji mkazi wa Unguja, na Nasorro Hamisi mkazi wa Zanzibar.
Amewataja majeruhi watano ambao wamekatika viungo vya miili yao, kuwa ni Njama Hassani, Fatuma Kesi, Sada Manga, na Twalibu, wote wamekatika mkono wa kushoto na mmoja mguu wa kulia, pamoja na Mohamed Daudi mkono wa kulia.
Aidha amesema majeruhi wengine 15 walitibiwa na kuruhusiwa, na hali zao zinaendelea vizuri, na kubainisha kuwa basi hilo lilikiwa na abiria 43 ambapo wengine ni wazima hawakuumia.
"Chanzo cha ajali hii ni mwendo kasi, ambapo Dereva wa basi anayejulikana kwa jina la Maxison Mkuru alishindwa kukata Kona na kusababisha ajali, na tunamsaka kwa sababu amekimbia," alisema Magiligimba.
“Miili ya Marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufani mkoani Shinyanga, na majeruhi wanaendelea na matibabu, na ninatoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani,”ameongeza.
Nao baadhi ya abiria waliokuwa kwenye basi hilo akiwamo Fotuna Wilbert, amesema baada ya kufika kwenye kona hiyo ya Didia basi likiwa katika mwendo kasi, walishaghaa kuona linayumba na kumshinda dereva na kupata ajali.
No comments:
Post a Comment