SERIKALI YAVIONYA VIWANDA VINAVYOCHAFUA MAZINGIRA. - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday 26 June 2021

SERIKALI YAVIONYA VIWANDA VINAVYOCHAFUA MAZINGIRA.

 


Serikali imeonya kukichukulia hatua kali za kisheria, Kiwanda chochote nchini kitakachobainika shughuli zake kushindwa kukabiliana na changamoto ya uchafuzi wa mazingira.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira),Selemani Jafo, katika ziara ya kushtukizia,kiwanda cha H & J Limited kinachozalisha mifuko ya viroba kilichopo Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani. 

Waziri Jafo alivitaka viwanda nchini kukabiliana na changamoto ya uchafuzi wa mazingira,katika maeneo yao ya uzalishaji bidhaa,na kudai hatakuwa tayari kukifumbia macho kiwanda chochote kitakachohusika na uchafuzi wa mazingira kwani Serikali inataka maendeleo yenye tija na yanayohifadhi mazingira.

Katika ziara hiyo ya ukaguzi wa Mazingira katika kiwanda hicho,alibaini changamoto mbalimbali za kimazingira ikiwemo utiririshwaji wa maji machafu kutoka kiwandani   na kwenda kwenye Mto Mbiki uliopo karibu na kiwanda hicho. 

 


Alisema changamoto nyingine,aliyoibaini kiwandani hapo,ni uchomaji wa mifuko inayotumia malighafi ya plastiki pamoja na wafanyakazi wa kiwanda hicho kutokuwa na vifaa vya kufanyia kazi.
 

sijaridhika na kiwanda hiki kinavyoendeshwa,niwatake NEMC kuja hapa na kufanya ukaguzi pamoja na kuchukua hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria ya mazingira,”alisema Waziri Jafo

Aidha alitoa miezi sita kwa kiwanda hicho kuweka mfumo wa uchujaji maji yanayotoka kiwandani kabla ya kwenda kwenye mazingira,ili kutoathiri uoto wa asili na kuleta athari katika jamii.

Kwa Upande wake Meneja wa Kanda ya Mashariki Kaskazini Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),Anorld Mapinduzi, alisema  kiwanda cha H& J ni kiwanda ambacho kimesajiliwa kwa kufuata taratibu za nchi. 

Alibainisha kuwa kiwnda hicho kilisajiliwa kwa ajili ya kupata cheti cha mazingira lakini mchakato wa upatikanaji wa cheti hicho haujakamilika na licha ya kulazimika kuanza kufanya shughuli zake. 

Mapinduzi alisema NEMC imepokea maelekezo,watafika  kufanya ukaguzi wa kina ili kuweza kuwachukulia hatua kulingana na sheria na kanuni ya Mazingira,kwakuwa imepewa imepewa mamlaka ya kusimamia mazingira,kwa maslahi ya Taifa. 

“.. hatupo tayari kuona wananchi wanaathirika kwa moshi, vumbi au kemikali zozote zile,” alisema Mapinduzi. 

Katika ziara hiyo Waziri Jafo pia alikagua kiwanda cha Keda Ceramic Limited kilichopo Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani kinachojihusisha na uzalishaji wa marumaru,na kuridhishwa na kinavyokabiliana na changamoto ya mazingira. 

Jafo alikipongeza kiwanda hicho kwa jinsi kinavyofanya shughuli zao bila ya kuchafua mazingira na kuwaomba wenye viwanda kuhakikisha wanafanya kazi zao bila ya kuathiri mazingira kwa maslahi ya Taifa.

 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso