EU YATAKIWA KUIONDOLEA VIKWAZO ZIMBABWE - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Thursday 17 June 2021

EU YATAKIWA KUIONDOLEA VIKWAZO ZIMBABWE




Na Mwaandishi Maalum, Dodoma
Tanzania imeendelea kutoa wito wa kuiondolea vikwazo vya kiuchumi Zimbabwe, ambavyo vimetajwa kuwa vinadumaza jitihada za nchi hiyo za kujiletea maendeleo. Wito huo umetolewa wakati wa Mkutano wa majadiliano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Ulaya (EU) uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 16 Juni 2021.

“Hakuna sababu ya kuendelea kuiwekea vikwazo Zimbabwe ilihali imefanya mabadiliko ya kimfumo katika maeneo mengi yakiwemo ya siasa, uchumi na mifumo ya sheria”, walisikika wakisema Mawaziri wa SADC, baada ya ujumbe wa Tanzania ambao uliongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) kuwasilisha hoja hiyo.

Ikijibu hoja hiyo, EU kupitia Waziri wa Mambo ya Nje wa Ureno, Mhe. Augusto Santos Silva ilisisitiza umuhimu wa Zimbabwe kuendelea kufanya mabadiliko katika mifumo yake na kudai kuwa vikwazo vilivyosalia havina athari yoyote kwa watu wa Zimbabwe. Ilisema, licha ya vikwazo hivyo, EU imeendelea kushirikiana na Zimbabwe kwa kuipatia misaada ya maendeleo na ya kibinadamu ambapo Euro milioni 366 na milioni 66 mutawalia zimetolewa kwa Zimbabwe katika kipindi cha miaka saba iliyopita.

Katika majadiliano hayo yenye lengo la kusaidia kukuza uchumi na maendeleo katika kanda ya SADC, Waheshimiwa Mawaziri walijadili kuhusu janga la UVIKO-19 na athari zake katika ukuaji wa uchumi na mikakati ya kujikwamua kiuchumi baada ya ugonjwa huo kudhibitiwa. EU iliahidi kuendelea kushirikiana na nchi za SADC kupitia programu mbalimbali zikiwemo za kuhakikisha kuwa kila mtu anapata chanjo na programu nyingine za unafuu wa kulipa madeni na misaada ya fedha za kukabiliana na athari za UVIKO-19.

Kuhusu mikakati ya kukabiliana na UVIKO-19, Nchi za SADC kupitia Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji, Mhe. Verónica Macamo alizihimiza nchi za EU kuzijengea uwezo nchi za SADC wa kutengeneza vifaa vya kukabiliana na UVIKO-19 badala ya kuagiza vifaa hivyo kutoka nchi zilizoendelea.

Kwa upande wa agenda ya hali ya siasa, ulinzi na usalama katika kanda ya SADC, Waheshimiwa Mawaziri walieleza kuwa hali ni ya kuridhisha, isipokuwa kumekuwepo na matishio na mashambulizi ya kigaidi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Msumbiji. EU iliahidi kuendelea kushirikiana na nchi hizo ili kukabiliana na changamoto za kiusalama katika Mashaiki ya DRC na jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji.

Nchi za SADC, zilitoa shukrani kwa misaada ya kiusalama inayopokea kutoka EU na kuzisihi nchi hizo kuendelea kutoa misaada hiyo kwa kuwa suala la ulinzi na usalama ni ndiyo moyo wa progarumu za ushirikiano wao kuendelea. Kutokana na umuhimu wa usalama katika kanda, EU iliombwa kuunga mkono mchakato wa uanzishaji wa Kituo cha Kukabiliana na Ugaidi cha SADC (SADC Regional Counter Terrorism Centre-RCTC).

Suala lingine lililojadiliwa na Waheshimiwa Mawaziri ni biashara na uwekezaji ambapo EU imepongeza jitihada zinazoendelea za kuwa na Soko Huru la SADC-EAC-ECOWAS na la Bara la Afrika (AFCFTA). Ilielezwa kuwa masoko hayo itakuwa chachu katika uwekezaji, ujenzi wa miundombinu, kuongezeka kwa ajira na kumaliza umasikini barani Afrika.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso