Asasi ya kiraia ya
wanawake Laki Moja Mkoani Shinyanga, ambayo inajishughulisha na kupinga matukio
ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto, pamoja na kupambana na umaskini
imezinduliwa rasmi leo.
PICHA: Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga
Zainab Telack, akizungumza kwenye uzinduzi wa Asasi ya Wanawake Laki Moja
Mkoani Shinyanga.
Uzinduzi huo umefanyika
katika ukumbi wa mikutano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, na
kuhudhuriwa na wanawake mkoani Shinyanga, Asasi za kiraia, Taasisi za kifedha,
Hakimu, Ofisa maendeleo, viongozi wa CCM, ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Mkuu wa
Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack.
Akisoma Risala kwa
mgeni rasmi,Katibu wa Asasi ya wanawake Laki Moja Mkoani Shinyanga Pendo Sawa,
amesema lengo la asasi hiyo ni kupinga matukio ya ukatili wa kijinsia kwa
wanawake, pamoja na kujengeana uwezo wa kuinuana kiuchumi.
PICHA: Meneja Biashara kutoka Benki
ya CRDB Mwanahamisi Iddi, akielezea fursa za wanawake zilizopo kwenye Benki
hiyo.
Amesema Asasi hiyo
ilianzishwa Mwaka 2020, na sasa imezinduliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga
kwa ajili ya kuendeleza mapambano ya kupinga matukio ya ukatili wa kijinsia
dhidi ya wanawake na watoto, vikiwemo vipigo, ubakaji, kulawiti, kutekeleza
familia zikiwemo mimba na ndoa za utotoni.
“Changamoto ambayo tumeiona sisi Asasi ya Wanawake Laki Moja juu ya kuendelea kwa matukio ya ukatili mkoani Shinyanga dhidi ya wanawake na watoto, ni tatizo la mila na desturi kandamizi, ambazo zimekuwa mwiba kwa jinsi ya kike na kuendelea kunyanyasika ndani ya jamii,”amesema Sawa.
“Kutokana
na changamoto hii ya kuendelea kwa matukio ya ukatili mkoani Shinyanga,
tunaomba Serikali ishirikiane na asasi za kiraia kutoa elimu kwa wananchi namna
ya kupambana na matukio ya ukatili ndani ya jamii, ikiwamo na kuzijua sheria ya
kupigania haki zao hasa kwa wanawake wajane ambao wamekuwa wakidhulumiwa mali
wanapofiwa na waume zao,”ameongeza.
Naye Mwenyekiti wa
wanawake Laki Moja Mkoani Shinyanga Annaskolastika Ndagiwe, ameeleza
kusikitishwa na matukio ya ukatili ambayo yanaendelea kutendeka mkoani
Shinyanga, huku wahusika wa matukio hayo wakishindwa kuchukuliwa hatua stahiki,
na kuendelea kuishi Uraiani kitendo ambacho amebainisha kinaumiza sana.
Amesema kuna baadhi ya
matukio ameshayatolewa taarifa kwenye mamlaka husika juu ya tukio la watoto
kufanyiwa vitendo vya ukatili, lakini cha ajabu wahusika wa matukio hayo hakuna
hatua zozote za kisheria ambazo zimechukuliwa juu yao, jambo ambalo linawapa
ugumu katika kuendeleza mapambano ya kupinga ukatili ndani ya jamii.
Kwa upande wake Mkuu wa
Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack, amewapongeza katika kuendeleza mapambano ya
kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, pamoja
na kuinuana kiuchumi.
Amesema Asasi hiyo ipo
katika muda muafaka, ambapo Mkoa huo unapambana na kutokomeza matukio ya
ukatili dhidi ya wanawake na watoto, na kuwataka wanawake hao watoe taarifa za
matukio ambayo wanafanyiwa watoto wao, pamoja na wao wenyewe, ili wahusika wachukuliwe
hatua kali za kisheria na kumaliza vitendo hivyo vya ukatili ndani ya jamii.
Telack amesema baadhi ya
wanawake wamekuwa hawatoi taarifa za matukio ya ukatili, kutokana na wahusika
wa vitendo hivyo kuwa ni ndugu zao wa karibu au waume zao, kwa kuhofia kuvunja
mahusiano, na kusababisha wahusika kutochukuliwa hatua, na vitendo hivyo vya
ukatili kuendelea kuwepo na hatimaye kuleta madhara baadae ikiwamo kupoteza
uhai, au mtoto kuambulia ujauzito.
Aidha amewaonya wazazi na
walezi kuacha tabia ya kuwalaza watoto chumba kimoja na wageni, bali wakalale
nao, na chumba hicho wamuachie mgeni, kwa sababu wageni wengine ndio wamekuwa
wahusika wakuu wa kuwafanyia watoto vitendo vya ukatili kwa kuwachezea michezo
michafu.
No comments:
Post a Comment