Na. Paul Kasembo, SHY RS.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amewashukuru na kuwapongeza Waheshimiwa Madiwani na Watumishi wa Manispaa ya Shinyanga kupitia viongozi wao Mstahiki Meya Mhe. Elias Masumbuko na Mkurugenzi Mwl. Alexius Kagunze kwa kuwa wamoja wakati wote.
Pongezi hizi amezitoa leo tarehe 1 Novemba, 2024 wakati akihutubia Baraza la Madiwani la Manispaa ya Shinyanga, ambapo amesema umoja wao, upendo, na mshikamano ndio umewawezesha kufanya kazi kama timu moja kwa kuwa kila upande una watu wake, huku akiwapongeza kwa kufanya hamasa ya kutosha wakati wa zoezi la kuandikisha wapiga kura.
“Niwapongeze sana nyote kwa kuwa wa kwanza kushirikiana na kudumisha upendo, umoja na mshikamano miongoni mwenu licha ya kwamba mnatoka pande tofauti lakini mmefanya kazi kubwa sana ya kuwahamasisha wananchi kujitokeza wakati wa zoezi la kuandikisha wapiga kura” amesema RC Macha
Akitoa salamu za Manispaa, Mstahiki Meya amesema kuwa wazipokea pongezi, shukrani na ushauri alioutoa RC Macha huku akimshukuru kwa kuwa karibu na Manispaa na kuahidi wataendelea kushirikiana bega kwa bega wakati wote katika kuwatumikia wananchi.
No comments:
Post a Comment