RC MACHA AWATAKA WANAFUNZI WA SHULE YA WASICHANA SHINYANGA SEKONDARI KUSOMA KWA BIDII, - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Wednesday 18 September 2024

RC MACHA AWATAKA WANAFUNZI WA SHULE YA WASICHANA SHINYANGA SEKONDARI KUSOMA KWA BIDII,



Na Paul Kasembo, SHY RS.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamiringi Macha amewaasa wanafunzi wa Shule ya Wasichana Shinyanga Sekondari kuweka jitihada na nguvu zote katika masomo ili kuhakikisha wanafanya vizuri na baadae waweze kutimiza ndoto na malengo waliyojiwekea ukizingatia Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewezesha kila kitu ikiwemo kuleta walimu, kujenga shule, kuweka miundombinu yote muhimu, kuleta vitabu, nishati ya umeme, maji na vingine vingi iliyobakia ni ninyi kusoma kwa bidii na ndiyo shukrani zenu pekee kwake Mhe. Rais.


Ameyazungumza hayo leo tarehe 18 Septemba 2024 alipotembelea shule hii akiwa ameambatana na Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamduni, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. Elias Masumbuko, Katibu Tawala Wilaya ya Shinyanga ndg. Said Kitinga, Mkurugenzi wa Manispaa Mwl. Alexius Kagunze na watalaam wengine.


Pamoja na ushauri huu, pia RC Macha ameipongeza sana Manispaa ya Shinyanga kwa usimamizi wa ujenzi wa shule hii ambayo inatajwa kuwa ya mfano kutokana na ubora, thamani yake pamoja na uahirikiano wao mzuri jambo ambalo linapelekea kukamilika kwa ujenzi huu ifikapo mwishoni mwa Septemba 2024.


“Ninawataka na kuwatia moyo sana ninyi wanafunzi wote katika shule hii, muelekeze bidii na jitihada zenu kubwa katika masomo yenu ili muhakikishe kwamba mnafanya vizuri na mnakuwa mfano wa kuigwa kwa wanafunzi wengine ambao watafuata baada yenu na pia kwa wanafunzi wa shule zingine na hatimaye muweze kuzifikia, kutimiza na kuziishi ndoto zenu pamoja na malengo mliyojiwekea ukizingatia Mhe. Rais wetu mpendwa amekwishaleta na kuwezesha kila kitu hapa” amesema RC Macha.


Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga CP. Hamduni amewataka watumishi wa Serikali mkoani Shinyanga kuwa makini katika kutekeleza kazi za Serikali, kutanguliza uzalendo na kuhakikisha kuwa thamani ya fedha inaonekana kwenye kazi zote na hasa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili iwe na tija iliyokusudiwa huku akisisitiza kwenda na kasi ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwahudumia na kuwaletea maendeleo wananchi wetu.


Akipokea ushauri huo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Mwl. Kagunze ameahidi kutekeleza kazi kwa viwango na kwa wakati ili kwenda na muda uliokusudiwa ambapo ujenzi wa shule hii unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Septemba 2024.


Aidha Kagunze ameongeza kuwa kufikia Januari 2025 Shule ya Wasichana Shinyanga Sekondari itakuwa tayari kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza ambao watakuwa wamechaguliwa hapo kwa kuwa miundombinu yote ya shule ipo tayari.


Kukamilika ujenzi wa Shule ya Wasichana Shinyanga Sekondari kunatajwa kusadia kwa kiasi kikubwa kuwawezesha wanafunzi wa Mkoa wa Shinyanga na Mikoa mingine kuwa na mazingira rafiki, mazuri na yenye kuvutia kwa kujisomea wanafunzi na kufundishia walimu kutokana na miundombinu bora iliyopo na kwamba hata thamani ya ardhi inaongezeka kutokana na uwepo wa shule hii.






No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso