TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA WAHASIBU AFRIKA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Wednesday 24 July 2024

TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA WAHASIBU AFRIKA



Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Pili wa Wahasibu Barani Afrika (African Association of Accountants General Meeting (AAAG)) utakaofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 3 hadi 5 Disemba Mwaka 2024, ukiwahusisha zaidi wa washiriki 2,000 kutoka takriban nchi 55 za Bara la Afrika.



Hayo yameelezwa na Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude, wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari jijini Arusha, uliolenga kuujulisha umma kuhusu mkutano huo na fursa za kiuchumi na kijamii kwa watanzania.



CPA Mkude alisema kuwa mkutano huo unatarajia kuleta manufaa makubwa kiuchumi na kijamii pamoja na kuitangaza sekta ya utalii ya Tanzania, hususan kwa wajumbe kutembelea vivutio vya utalii vilivyoko katika ukanda wa Kaskazini.



Alizitaja faida nyingine za mkutano huo kuwa ni pamoja na kuwa na Afrika yenye mafanikio yenye msingi wa ukuaji jumuishi na maendeleo endelevu, Bara jumuishi lililounganishwa kisiasa na kwa kuzingatia maadili ya Pan-Africanism.



Aliyataja manufaa mengine kuwa ni pamoja na kuwa na maono ya Mwamko wa Afrika na Afrika yenye utawala bora, demokrasia, kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria, Afrika yenye amani na usalama na Afrika yenye utambulisho thabiti wa kitamaduni, urithi wa pamoja na maadili.



CPA Mkude alisema kuwa Mkutano huo utawaleta Wahasibu wakuu wa Serikali Afrika watakaoambatana na Wahasibu Wakuu wa Wizara, Taasisi za umma na Wahasibu na wadau wengine ambao watapata fursa ya kusikiliza mada za masuala mbalimbali ya kitaaluma na kubadirishana mawazo na kujua fursa zinazopatikana katika nchi za Afrika.



Alisema wageni kutoka nje watakuja na fedha za kigeni ambazo watazitumia hapa Tanzania kwa kuwa watatembezwa kwenye mbuga za Wanyama na vituo mbalimbali vya utalii na hivyo kuunga mkono dhamira ya Mheshimiwa Rais ya kuutangaza Utalii wa Tanzania.



Alitoa wito kwa wafanyabiashara wa nyumba za wageni (hoteli), usafiri, mamalishe na jamii kwa ujumla kuchangamkia fursa hiyo ya ujio wa wageni ili kunufaika kiuchumi na kijamii.



“Natoa wito kwa Maafisa Masuuli wa Wizara na Taasisi zote kuwaruhusu Wahasibu, wakaguzi na wadau wengine watakaoomba kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Pili wa Wahasibu wakuu wa Serikali Afrika, African Association of Accountants General (AAAG) utakaofanyika jijini Arusha mwezi Desemba, 2024”, alisema CPA Mkude



Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Wahasibu wa Afrika, ambaye pia ni Mhasibu Mkuu wa nchi ya Lesotho, Bi. Malehlohonolo Mahase, alisema Mkutano wa Wahasibu Afrika unafanyika Tanzania kwa kuwa ni mwanachama anayeaminika na amekuwa mshiriki mwaminifu katika umoja huo, na kwamba wajumbe wa mkutano huo wanakuja kujifunza namna Tanzania ilivyopiga hatua kubwa katika matumizi ya mifumo ya fedha.



Alisema kuwa Tanzania ipo vizuri katika kutekeleza viwango vya kimataifa vya kihasibu, imekuwa ya mfano katika ukuaji wa Uchumi, imeimarika katika suala la ukarimu wa wageni, maendeleo katika teknolojia ya Habari na Mawasiliano na ni miongoni mwa nchi zenye vivutio vingi vya utalii hivyo wanachama kuna mambo mengi ya kujifunza.



Aidha alieleza kuwa Mkutano huo utakao wakutanisha pia Jumuiya za wafanyabiashara watapata fursa ya kujua ni namna gani Afrika ipo tayari katika suala la uwekezaji na namna ya kuripoti hali ya Uchumi ya Afrika, jambo ambalo litaongeza uwazi na uwajibikaji.



Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), Bi. Christine Mwakatobe alisema kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha wageni wanapokuja wanapata huduma bora kwa kuwa wanaamini watakuwa mabalozi wa Tanzania na watatembelea vivutio mbalimbali vya utalii.



Alisema anamshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuitangaza nchi yetu Duniani na kwamba hauo ni matunda ambayo Taasisi za Serikali kwa ujumla zinafaidi kwa kazi yake anayoifanya, huku Kituo chake cha Mikutano kikihudumia mikutano mingi ya Kitaifa na Kimataifa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso